Tuesday, January 3, 2012

SUMAYE AUNGANA NA ZITTO KABWE..APONDA POSHO MPYA ZA WABUNGE


  • Ni hoja iliyoasisiwa na kuvaliwa njuga na Zitto kabwe.  


    WAZIRI Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye amezungumzia mwelekeo wa taifa huku akionya kuwa nyongeza za posho zisizofuata utaratibu kwa watumishi wa umma ni hatari na ni utawala mbaya kwa nchi.Alisema suala la posho ni jambo ambalo sasa limekuwa tatizo kwa Serikali na kuwa imefika wakati ofisi za Serikali zimehamia hotelini lengo likiwa ni watumishi wa umma kutafuta mwanya wa kulipana posho.

    “Ndiyo maana watu wa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) wanakusanya fedha nyingi, lakini ni fedha kidogo sana zinazokwenda kwenye huduma za jamii. Nadhani hili ni tatizo na ni utawala mbaya kabisa, lazima kuwepo mabadiliko kama kweli tunataka kuisaidia nchi yetu,” alisema Sumaye.
    Kuhusu posho za wabunge, Sumaye alisema ni jambo la hatari kwani ikiwa wabunge watalipwa viwango vya posho vilivyotangazwa, linaweza kuvuruga amani ya nchi.

    Sumaye alisema hayo katika kipindi cha dakika 45 kinachotushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV. Alisema ongezeko la posho za wabunge linaweza kuchochea makundi mengine kudai akitolea mfano wa wanajeshi, polisi, Mahakama na walimu jambo ambalo alisema litamweka Rais katika wakati mgumu kufanya uamuzi.

    “Mwanasiasa mzuri akifanya jambo akiona limewaudhi wananchi anatakiwa aliache, lakini pia kwenye hili, huu mkanganyiko wa Spika na Katibu wake na huu ukimya wa Ikulu ni tatizo. Tungependa waseme ili umma ujue hali ikoje,” alisema Sumaye.  Alisema hatua ya Bunge kujipandishia posho ya kikao kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 kwa siku haliingii akilini na kwamba linakiuka utaratibu uliowekwa na Serikali katika kulipa gharama kwa maofisa wake ikiwa gharama hizo ni zaidi ya kiwango cha fedha za kujikimu zilizowekwa.

    “Siyo kwamba napinga posho. Wabunge wanastahili posho, lakini kwa kweli kujiongezea kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 siyo sahihi,” alisema Sumaye.Alisema wakati alipoteuliwa na Rais Benjamin Mkapa kwa Awamu ya Pili kushika wadhifa wa Waziri Mkuu, aligoma kwa sababu alikuwa amekwaruzana na wabunge kuhusu nyongeza ya posho.

    “Nilimwambia wabunge watanikataa kwa sababu nimegombana nao sana juu ya suala la posho lakini akasema lazima uwe na mimi ndipo nikakubali. Lazima hili suala liangaliwe mara mbilimbili, leo wabunge mmejiongezea kesho jeshi, polisi na walimu nao watataka, tutafanyaje? Tusifanye mambo ambayo yatamuweka Rais pabaya,” alisema

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...