Saturday, March 31, 2012

Lowassa: Mimi mtu wa vitendo,porojo sitak


HATIMAYE Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa amepanda jukwaani kumpigia debe mgombea ubunge wa CCM katika uchaguzi mdogo Jimbo la Arumeru Mashariki, Sioi Sumari, akiwaambia wananchi wa jimbo hilo kuwa Sioi ni mchapakazi na siyo mtu wa blah blah na kwamba atawatatulia kero zao ikiwemo ya maji.
Kupanda jukwaani na kumnadi Sioi kumemaliza mjadala wa kama Mbunge huyo wa Monduli (CCM), angepata fursa hiyo kutokana na kile kilichokuwa kimeelezwa kuwa ni mgawanyiko mkubwa uliopo ndani chama hicho.
Awali, kulikuwa na taarifa kuwa Lowassa alikuwa hatakiwi kupanda jukwaani kumnadi mgombea huyo kwa maelezo kuwa kufanya hivyo kungekiharibia zaidi chama hicho.
Jana Lowassa alitengua kitendawili hicho saa 7:07 mchana alipowasili kwenye Viwanja vya Kikatiti akiwa na msafara wa magari yasiyopungua 20 yakiongozwa na pikipiki.
Baada ya kufika alipanda jukwaani kwa staili ya kukimbia na baadaye kucheza muziki jukwaani na kushangiliwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Akihutubia, Lowassa alisema wakazi wa jimbo hilo wanamfahamu kwamba yeye si mtu wa maneno, bali vitendo hivyo kwa kumchagua Sioi, ajenda ya maji itafungwa baada ya mgombea huyo kuapishwa.
Lowassa pia alimwagia sifa, Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kuwapatia wakazi wa Kata ya Nduruma, Arumeru eneo la ekari 5,000 akisema ni mchapakazi hodari anayestahili heshima.
Alikipiga vijembe Chadema akisema kilisababisha maandamano na vurugu katika Jimbo la Arusha Mjini na kuufanya mji huo kutokalika na kuwataka wakazi wa Arumeru wasikichague.
Alisema endapo watamchagua mgombea wa Chadema watakuwa wamefungulia fujo katika jimbo hilo kuanzia Mto Nduruma kuingia wilayani mwao.
Lowassa aliipongeza Kamati Kuu ya CCM kwa kupitisha jina la Sioi kuwania ubunge wa jimbo hilo akisema chama hicho kimeonyesha ukomavu wa demokrasia.
Alisema amekwenda Arumeru kumpigia debe Sioi kwa kueleza sera zinazotekelezeka na si matusi... “Sasa nimekuja kumpigia debe mgombea wetu, lakini debe nililokuja nalo si debe la matusi. CCM haina chuo cha matusi wanaoningoja nitukane sina matusi.”
Akimnadi Sioi, Lowassa alisema kwa kumchagua, wakazi hao watakuwa wanafunga mjadala wa kero ya mashamba na ardhi kwa ujumla katika jimbo lao kwa kuwa litafikishwa kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili litatuliwe.
“Kwa uchaguzi huu tunafunga ajenda ya matatizo ya ardhi na mashamba Arumeru. Jumapili mkimchagua Sioi kuwa mbunge wenu tunafunga ajenda ya matatizo ya ardhi nawaambieni,” alisema Lowassa.
Alisema tayari Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye ameshafanya ziara katika jimbo hilo na kuorodhesha mashamba yote yenye matatizo, hivyo yuko njiani kufikisha jalada hilo mbele ya Rais Jakaya Kikwete kwa lengo la kupatiwa ufumbuzi.
“Lazima nikiri kuwa hatukulishughulikia vya kutosha suala la ardhi lakini kwa uchaguzi huu, tunafunga agenda ya matatizo ya ardhi Arumeru Mashariki kama mtatupa Sioi Sumari tufanye naye kazi,” alisema Lowassa.
Aliwananga mahasimu wake wa kisiasa wanaoeneza maneno kwamba amekwenda kumpigia debe Sioi kwa kuwa ni mkwe wake na kusema hakuna dhambi kwa mkwewe huyo kugombea jimbo hilo kwa kuwa anazo sifa… “Hata mkisema ni mkwe wangu, kwani kuna dhambi gani? Alimpenda Pamela sasa nimkatae kwa kuwa mimi ni mwanasiasa?”
Lowassa aliwataka wananchi wa jimbo hilo kumchagua mgombea wa CCM kwa kuwa ni chama pekee kinachubiri na kutetea amani ya nchi na kusema Jiji la Arusha sasa halikaliki kutokana na vurugu na maandamano yasiyokwisha.
Alihoji iweje vurugu hizo ziwepo katika Jiji la Arusha tu wakati katika majimbo ya Karatu, Moshi Mjini na Hai yanayoongozwa na Chadema hali ni shwari?
“Anayejiandaa kuwapa kura hao (Chadema) anasogeza vurugu kutoka Arusha mjini hadi Patandi na Kikatiti ni lazima mtafakari sana… hata mkisema Sioi ni mkwe wangu kwani kuna tabu gani?... naomba mchagueni awe Mbunge” alisema.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...