Wednesday, June 20, 2012

MKUTANO WA MASHOGA WAVUNJWA NA POLISI

Polisi wa Uganda wazuia mkutano wa mashoga

Hii ni mara ya pili kwa serikali ya Uganda kuwazuia mashoga kukusanyika, mara ya kwanza walizuia mkutano kama huo mwezi Februari
Wapenzi wa jinsia moja katika nchi nyingine duniani
Picha ASSOCIATED PRESS
Wapenzi wa jinsia moja katika nchi nyingine duniani
Polisi nchini Uganda Jumatatu  jioni waliivunja warsha ya siku tatu ya wapenzi wa jinsia moja wakisema mkutano huo ulikiuka sheria kwa sababu wapenzi wa jinsia moja hawatambuliwi na sheria. Watu wanne akiwemo waandalizi wa mkutano huo walitiwa mbaroni.

Mkutano huu ulikuwa unahudhuriwa na washirika 20 kutoka nchi ya Rwanda, Tanzania, Kenya na Uganda. Kila nchi ikiwa imechangia washiriki watano.

Njoroge Waithera kutoka Kenya ni miongoni mwa watu waliokuwa wanahudhuria mkutano huu.

Mwandishi wa Sauti ya Amerika alimuuliza kama mkutano huu ulikuwa wa wapenzi wa jinsia moja.

Waithera alijibu “ Hapana, La hasha kwa sababu mimi mmoja wa washiriki, mimi nimeoa, niko na bibi na niko na watoto watatu, hii ni warsha ya mafunzo ya kuweza kunakili ukiukaji wa haki za binadamu na mimi nimekuja kwa sababu ya ule ujuzi wangu wa kuweza kunakili na kufanya uchunguzi wa haki za binadamu na hilo ndio jambo ambalo tulikuwa tunafunza watu hapa kufanya na tuko na watu kutoka nchi tofauti ili nao wakirudi makwao wanaweza pia kufunza watu wengine jinsi ya kunakili haya matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu ili tuweze kuwa na ushahidi hata kama ni  wakati ule tunataka kupeleka kesi kortini ama kufanya ile advocacy kuishinikiza serikali ziweze kushughulikia mambo fulani tuwe na ushahidi wa kutosha. “

Waziri wa maadili Simon Lokodo ambaye aliamrisha kuvunjwa kwa warsha hii na kukamatwa kwa washiriki hakukubaliana na maelezo yaliyotolewa na Njoroge. Alisema alikuwa na habari kuwa  “wapenzi wa jinsia moja pamoja wa watu wengine waliokuwa wametoka ng'ambo wamekuwa wakikutana ili kupeana motisha na kuhalalisha kuwepo kwao hapa nchini.”

Miongoni mwa waliokamatwa ni wakenya wawili, mganda mmoja na mzungu mmoja ambaye uraia wake haukuweza kupatikana mara moja.

Hii ni mara ya pili kwa waziri wa maadili nchini Uganda, Simon Lokodo kuuvunja mkutano wa mashoga. Mara ya kwanza mkutano ulivunjwa mwaka huu mwezi wa pili mjini Entebbe.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...