Matokeo ya uchaguzi yahairishwa Misri
Tangazo la matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika mwishoni
mwa wiki limehairishwa, hii ni kulingana na taarifa kwenye televisheni ya
kitaifa.
Matokeo hayo yalikuwa yatangazwe alhamisi, lakini tume ya uchaguzi
imelazimika kuhairisha tangazo hilo ili kushughulikia malalamiko yaliowasilishwa
na wagombea.
Wagombea hao Mohammed Mursi na Ahmed Shafiq wote wamedai kushinda uchaguzi
huo.
Kulingana na tume ya uchaguzi jumla ya malalamiko 400 yamewasilishwa lakini
haijasema matokeo hayo yatatangazwa lini.
Msemaji wa vuguvugu la Muslim Brotherhood, Nader Omran amesema kuwa tangazo
hilo halifai kuhairishwa.
"Hatua hii itachochea hali ya wasiwasi itakuwa bora zaidi suala hili
limalizwe alhamisi" amesema Bw Omran.
Wasimamizi wa kampeni ya mgombea wa Muslim Brotherhood, Mohammed Mursi
wanasema kuwa kura zinaonyesha kuwa alishinda duru hiyo ya pili ya uchaguzi.
Lakini mshauri wa karibu wa Ahmed Shafiq, amewaelezea waandishi wa habari
mjini Cairo kuwa, Shafiq- aliyekuwa waziri mkuu chini ya Utawala wa rais Hosni
Mubarak-alishinda uchaguzi huo.
Maelfu ya watu wamekusanyika katika bustani ya Tahriri tangu juzi kulaani
baraza kuu la jeshi ambalo juzi limejilimbikizia mamlaka baada ya mahakama kuu
kulivunja bunge la nchi hiyo.
BBC.
No comments:
Post a Comment