Friday, December 30, 2011

UBUNGE WA KAFULILA

Profesa Safari: Kafulila bado mbunge
WAKATI upepo ndani ya NCCR-Mageuzi ukigeuka ghafla baada ya Mahakama Kuu kutoa amri ya kuzuia uamuzi wa chama hicho kumvua uanachama mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, Profesa Abdallah Safari amesema amri hiyo ni ya kawaida na inamaanisha kuwa mbunge huyo ataendelea na shughuli za kibunge.

Majonzi ya Kafulila yalibadilika baada ya Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam kutoa amri kwa uongozi wa NCCR-Mageuzi ukiitaka usiendelee na utekelezaji wa uamuzi wa Nec yake ya Desemba 17 iliyomvua uanachama Kafulila na wenzake watatu hadi kesi ya msingi namba 218/2011 itakapomalizika.

Akizungumza Dar es Salaam jana Profesa Safari ambaye kitaaluma ni mwanasheria alisema, “Ninavyojua ni kwamba amri hiyo imetolewa na mahakama na huyo Mbunge (Kafulila) ataendelea kuhudhuria shughuli za Bunge mpaka kesi hiyo ya msingi itakapomalizika”.

Alifafanua kuwa amri hiyo imelenga kuzuia maamuzi ya NCCR-Mageuzi hadi kesi ya msingi iliyofunguliwa na Kafulila itakapomalizika.Profesa Safari alisema jambo hilo ni la kawaida katika masuala ya sheria huku akisisitiza kuwa kesi itakapomalizika ndio hatua nyingine zinaweza kufuatwa.

Gazeti hili lilimtafuta Spika wa Bunge, Anne Makinda ili kutoa ufafanuzi wa Ofisi ya Bunge kuhusu nafasi ya Kafulila lakini simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila majibu.Pia Katibu wa Bunge Thomas Kashililah pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge, John Joel walisema kuwa hawawezi kulizungumzia suala hilo kwa kuwa wako nje ya ofisi bila kufafanua ni lini wataweza kulitolea ufafanuzi suala hilo.

Juzi NCCR kiliitisha mkutano na waandishi wa habari huku kikitumia muda mwingi kulaumu uamuzi wa Kafulila kupeleka suala hilo mahakamani.Mkuu wa Idara ya Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa chama hicho, Dk Sengondo Mvungi alisema kuwa wameshangazwa na zuio hilo la Mahakama kwa kuwa Kafulila alikuwa amemwandikia barua mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia akiomba Nec irejee upya uamuzi wake wa kumvua uanachama.

“Wakati chama kikijadili suala hili, Kafulila aliwasilisha malalamiko yake kwa Msajili wa Vyama vya Siasa Desemba 19, na Msajili alituandikia barua juu ya malalamiko ya Kafulila na barua yake tuliipata Desemba 27,”alifafanua Dk Mvungi.Aliongeza, “Kabla ya kutafakari hatua za kufanya kuhusu mambo hayo mawili, tumepokea hati ya Mahakama jana (juzi) jioni.”

Akizungumzia msimamo wa chama hicho Dk Mvungi alisema uamuzi wa Nec bado haujatenguliwa wala kujadiliwa na kwa amri hiyo ya Mahakama, sasa hawatafanya chochote zaidi ya kuacha uamuzi huo uendelee kama ulivyo.

“Ufafanuzi zaidi wa kilichoamriwa na mahakama ni kuhusiana na yale waliyoyaomba ambayo, hakuna hati yoyote inayoonyesha maombi ya kubatilisha uamuzi wa Nec,” alisema Mvungi.

Hata hivyo, alifafanua kwamba suala la kuamuru upande wao katika kesi usifanye jambo zaidi ni  mamlaka ya makakama na kwamba, chama hicho hakina tatizo na suala hilo.Alisema kinachotakiwa kueleweka ni kuwa mahakama haijatoa amri ya kuwabakiza waliovuliwa uanachama katika chama,  wala hakuna amri ya kuwafutia adhabu yoyote waliyopewa wale walioadhibiwa.

Alisema uamuzi wa Nec ya chama hicho unabaki kuwa sahihi na halali kwa mujibu wa sheria za nchi, mpaka pale ambapo mahakama itakapoamua vinginevyo.Dk Mvungi ambaye ni mwanasheria aliyebobea katika masuala ya Katiba, alisema  chama hicho hakikushirikishwa na mahakama katika uamuzi wake wa kutoa zuio.

“Sijui walimshauri vipi huyo Jaji na sisi ilitakiwa tupate tusikilizwe, jaji aliwasikiliza bila kuwataka wawasiliane na sisi (NCCR).”

Alihoji kwamba kama Kafulila na wenzake walilalamika kuwa hawakupewa haki ya kujieleza na Nec, hata mahakama kuu nayo haikuwapa nafasi ya kuwasikiliza walamikiwa ambao ni Mbatia na NCCR.“Katika hili NCCR na Mbatia hawakupewa haki ya kusikilizwa kwa kuwa ndio walalamikiwa, sio kweli kwamba Mahakama Kuu umempa ushindi Kafulila katika shauri dhidi ya chama” alisisitiza.
                                                                   MWANANCHI

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...