Thursday, January 5, 2012

Mapigano yazuka kati ya wapiganaji Libya

Mapigano yazuka kati ya brigedi ya wapiganaji mjini Tripoli
Watu wanne wameuawa na wengine watano kujeruhiwa katika majibizano ya risasi yaliyozuka mapema katikati ya mji mkuu wa Libya, Tripoli.
Yalitokea katika jengo moja la kijasusi lililopigwa na NATO mwaka jana yalipozuka mapinduzi ya kiraia dhdi ya kiongozi Muammar Gaddafi.
Brigedi moja kutoka mji wa Misrata ilijaribu kuwaachilia huru wafungwa, na kuanzisha mzozo na kundi lingine lililokuwa na silaha kutoka Tripoli.
Majeruhi walitoka pande zote mbili.
Milio ya risasi ilisikika karibu na jengo hilo kati ya mitaa ya Zawiya na Said.
Barabara zilifunguliwa haraka mara baada ya hali hiyo kutulizwa.
"Nasikitika kwa tukio hilo. Sitaki kuingia kwa undani zaidi, lakini ilikuwa ni matokeo ya matatizo kati ya wanamapinduzi wa Misrata na wanachama wa baraza la kijeshi la mtaa wa Zawiya ," Abdul Hakim Belhaj, mkuu wa baraza la kijeshi la Tripoli aliuambia mkutano wa waandishi wa habari.
"Kilichotokea ni kitendo cha kizembe na hali sasa imedhibitiwa. Tangu mchana hatujasikia tena milio yoyote ya risasi," alisema.
Ilikuwa ni dalili nyingine ya tishio kwa usalama linalosababishwa na wapiganaji waliokata tamaa wanaojaribu kuachana na hadhi ya uasi, anasema mwandishi wa BBC Mark Lowen akiwa Tripoli.
Bado wana nguvu kutokana na kutokuwepo kwa jeshi la kitaifa au polisi.
Lakini serikali mpya ya Libya chini ya shinikizo, sasa imeanza mchakato wa kuyashunghulikia makundi na kuyaunganisha na wizara za ulinzi na mambo ya ndani, mwandishi wa BBC anasema.
Makumi ya maelfu ya wapiganaji bado yako kwenye brigedi mbalimbali, na kumezuka mfululizo wa mapaigano kati yao katika wiki za hivi karibuni.
Mabadiliko kutoka vita vya wenyewe kwa wenyewe kuingia kwenye usalama na Libya iliyotulia bado ni hatua ya taratibu na ngumu na tatizo la kushughulikia wapiganaji ni mojawapo ya changamoto zilizo mbele, mwandishi wa BBC anaongeza.
BBC

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...