Thursday, December 29, 2011

CHUPU CHUPU JAHAZI LISABABISHA VILIO

WATU 13 wameokolewa wakiwa hai baada ya jahazi walilokuwa wakisafiria kugonga mwamba na kuzama katika eneo la Nyororo lililoko Bahari ya Hindi.Ajali hiyo ilitokea Jumatatu wiki hii saa 3:30 usiku katika eneo hilo lililoko katikati ya Bahari ya Hindi.

Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) David Mziray alisema jana kuwa watu wanane wakiwamo waathirika wa ajali hiyo wamepatikana Mafia wakiwa hai na kufanya idadi ya waliokolewa kufika 13.

Alisema jahazi hilo lilikuwa linakisiwa kuwa na watu kati ya 20-25 na kwamba juhudi za kuwatafuta watu wengine, zinaendelea.Alisema Jumatatu wiki hii kituo cha uokoaji na utafutaji cha Dar es Salaam (MRCC), kinachoendeshwa na Sumatra kilipokea taarifa ya kutokea kwa ajali ya Jahazi ya Zulkani.“Zulkani haikuwa na usajili rasmi na ilikuwa safarini kutoka kisiwa kidogo cha Jibondo-Mafia kuelekea Dar es Salaam,”alisema Mziray.

Alisema taarifa za ajali hiyo zilitolewa na Amani wa African shipping LTD  ambaye alipigiwa simu na ndugu yake Juma aliyekuwa anasafiri na jahazi hilo .
Alisema baada ya taarifa hizo kituo cha MRCC kiliwasiliana na Juma ambaye alikuwa mmoja wa watu waliookolewa.
Alisema Juma alitoa maelezo kuwa waliondoka Jibondo-Mafia saa 12:00 jioni Desemba 26 kuelekea Dar es salaam na walipofika Nyororo walipigwa na dhoruba iliyosababisha jahazi kugonga  mwamba na hatimaye kuzama.

Kwa mujibu wa Mziray, Juma na wenzake wanne walifanikiwa kuokolewa na jahazi la wavuvi.
Alisema kituo cha MRCC kilitoa taarifa kwa Jeshi la wanamaji (Navy), Polisi wanamaji (Police Marine), Mwakilishi wa Bandari Mafia na  Mwakilishi wa Sumatra Mafia.
Katika hatua nyingine Sumatra imesema haitavisajili vyombo vya usafiri vinavyozidi miaka 10 ili kutunza mazingira.

Mamlaka hiyo ilisema vyombo vingi vinavyoingizwa nchini ni chakavu na kwamba vimesababisha uharibifu wa mazingira na kufanya Tanzania kuwa dampo la magari chakavu.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...