Thursday, December 29, 2011

SAKATA LA KAFULILA BADO TETE- NCCR WATOA TAMKO


David Kafulila  

AMRI ya Mahakama Kuu iliyozuia utekelezaji wa uamuzi wa Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi kumvua uanachama Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila imeonekana kuuchanganya uongozi wa chama hicho ambao jana ulilazimika kutoa ufafanuzi wa hatua hiyo ukisema haujatengua uamuzi wake huo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Idara ya Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa chama hicho, Dk Sengondo Mvungi alisema kabla ya kupokea hati ya Mahakama Kuu juzi juu ya amri hiyo, simu za wanachama wake mbalimbali pamoja na mitandao ya kijamii imekuwa ikiandika habari kuwa mahakama hiyo tayari imempa Kafulila ushindi katika shauri lake dhidi ya chama hicho.

“Msimamo wa chama kwa sasa ni kwamba maamuzi yake ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Desemba 17, mwaka huu bado hayajatenguliwa wala kujadiliwa na mahakama yoyote ile. Isipokuwa kwa sasa tumepokea amri ya Mahakama Kuu ikizuia chama kisiendelee na hatua zaidi dhidi ya Kafulila na wenzake walioshiriki kushtaki chama kwenye kesi namba 218 ya mwaka 2011 mpaka shauri la msingi litakapoamuriwa,” alisema na kuongeza:

“Ufafanuzi wa kilichoamriwa na mahakama ni kuhusiana na yale waliyoyaomba ambapo hakuna hati yoyote inayoonyesha maombi ya kubatilisha maamuzi ya Halmashauri Kuu ya Taifa (ya NCCRR-Mageuzi). Suala la kuamuru upande katika kesi usifanye jambo zaidi ni katika mamlaka ya mahakama ambalo chama hakina tatizo na suala hilo.”

Hata hivyo, Dk Mvungi alisema hakuna amri yoyote ya mahakama iliyotolewa ya kuwabakiza waliovuliwa uanachama katika chama huku akisema suala la ubunge wa Kafulila lipo mikononi mwa Spika wa Bunge na kwamba wao kama chama nguvu yao inaishia katika kumvua uanachama.

Kauli ya Bunge

Akizungumzia suala hilo, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai aliliambia gazeti dada la Mwananchi, The Citizen kwamba mahakama haiwezi kuiandikia barua Bunge kulitaka lisitoe uamuzi kuhusu Kafulila.

Alisema Mahakama inaweza kuiandikia barua NCCR na kuitaka iliandikie Bunge barua kusitisha utekelezaji wa suala lake.

Alipoulizwa kama Bunge litaendelea na taratibu za barua ya NCCR ya kumvua uanachama Kafulila, Ndugai alisema: “Bunge litaendelea na taratibu zake kama kawaida.”

Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi, ilimvua uanachama Kafulila, Desemba 18, mwaka huu, siku 10 baada ya kumwengua kwenye nafasi ya Katibu Mwenezi wa chama hicho kwa tuhuma za kutoa siri za chama.

Baada ya uamuzi huo, Kafulila aliandika barua kwa Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia akiomba kikao cha Halmashauri kuu kiitishwe tena kurejea uamuzi wake na baadaye kuwasilisha malalamiko yake kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye alikiandikia chama hicho barua kutaka ufafanuzi wa malalamiko ya mbunge huyo kisha alikwenda Mahakama Kuu kuomba amri ya kuzuia utekelezaji wa uamuzi dhidi yake baada ya kufungua kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama. MWANANCHI
   

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...